Kila mwezi, Baba Mtakatifu huukabidhi Mtandao wake wa Sala Ulimwenguni nia za sala. Nia hizi hutuelekeza kujiunga naye katika kujali utu na utume wa Kanisa. Nia hizi ni wito kwa ulimwengu wote kuziweka sala zetu katika matendo mahsusi; ni dira ya utume wa huruma kwa ulimwengu. Kwa kupitia mpango huu sote tunahamasishwa kutumia sala na matendo mema kujenga ulimwengu wenye utu na mapendo zaidi. Pia tunaunganishwa kujenga tabia binafsi na za kijumuiya ya kuleta mabadiliko chanya ulimwenguni.
Baba Mtakatifu anapotupa nia zake za sala anatusaidia kuwa karibu na Moyo Mtakatifu wa Yesu, na kuutazama ulimwengu kwa Macho ya Kristo yenye huruma na upendo. Hii huwezekana kwa kukubali upendo na huruma ya Mungu kujaza mioyo yetu kwa sala na Tafakari ya Upendo wake, kisha kwa maisha yetu kuacha kwa makusudi upendo huu kusambaa kwa wengine na kuleta mabadiliko mema ulimwenguni.
Soma au pakua waraka rasmi wa Nia za Sala za Baba Mtakatifu kwa mwaka 2026.
Pakua PDFVideo ya Papa ni mradi rasmi wa Baba Mtakatifu unaowasilisha sala yake ya kila mwezi, inayohusiana na nia ya sala ya mwezi huo. Mpango huu ulianza mwaka 2016, na kwa sasa una watazamaji zaidi ya milioni 260 katika mitandao mbalimbali ya kijamii ya Vatican. Ikiwa inatafsiriwa katika lugha zaidi ya 23 katika nchi 114, Video ya Papa huwasaidia watu kujiunga na Baba Mtakatifu katika kuzisalia nia zake. Kwa maneno mengine, video hii ni mwaliko wa Papa kwa watu wote duniani kusali, kutafakari na kutenda pamoja naye.
Tembelea tovuti rasmi ili kupata video mpya ya mwezi.
Nenda tovuti rasmiKufanya afya ya akili kuwa sehemu ya huduma ya kichungaji
Tujijengee namna ya kuelewa, kutunza, na kutoa tumaini kwa wenye changamoto za akili. Maumivu ya ndani mara nyingi huwafanya wahanga wake kujitenga, kunyamaa au kuwa na hofu. Lakini tunaweza kuungana nao kwa njia ya kuwajali: neno la upole, sikio linalosikiliza, au sala ya kimya.
Huduma ya afya ya akili si jukumu la wataalamu pekee; ni jukumu la wote. Kama Kanisa tunapaswa “kuwakumbatia”, kuwaelewa, na kuandamana na wenye changamoto za afya ya akili. Jamii yenye kukaribisha tayari ni dawa kwa roho. (Rejea Hatua ya 8 na 9 za Njia ya Moyo: Utume wa huruma kwa ulimwengu. Mtandao wa kimataifa wa sala na huduma.)
Ee Baba mwema, natambua uko hapa pamoja nami.
Nakuja mbele yako katika siku hii mpya.
Weka moyo wangu kwa mara nyingine tena karibu na Moyo wa Mwanao Yesu,
anayejitoa kwa ajili yangu na anayekuja kwangu katika Ekaristi.
Roho wako Mtakatifu anifanye kuwa rafiki na mtume wake, aliye tayari kwa utume wake wa huruma ulimwenguni.
Ninaweka mikononi mwako furaha na matumaini yangu, kazi zangu na maumivu yangu, mimi mzima na kila kitu nilichonacho,
kwa kushirikiana na kaka na dada zangu wa Mtandao huu wa Sala Ulimwenguni.
Pamoja na Mama Maria, ninakutolea siku yangu kwa ajili ya utume wa Kanisa na kwa nia ya Sala ya Baba Mtakatifu [na Askofu wangu] kwa mwezi huu.
Amina.
Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amina.
Mungu wa uzima,
Unajua mioyo yetu kwa ndani kabisa, unajua nuru na giza vilivyomo ndani yetu, na majeraha ya siri ambayo wakati mwingine hakuna anayeyaona.
Leo tunawaleta mbele yako ndugu zetu wanaopambana na changamoto za afya ya akili, wanaoteseka peke yao kwa wasiwasi, sonona, au aina nyingine ya ugonjwa wa akili.
Kwa upole, unawaita kwa majina, na ndani yako wanarudishiwa tena utu na tumaini.
Ee Bwana, tusamehe kwa nyakati tulipowageuzia kisogo wenzetu hawa, tukichochea unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya wenye matatizo ya afya ya akili.
Lifanye Kanisa lako liwe nyumba iliyo wazi, mahali salama ambapo kila mtu anapata nafasi — jumuiya inayoandamana na kila mtu na isiyomtenga yeyote, inayosikiliza bila kuhukumu na inayokwenda karibu na wote bila hofu.
Tunakusihi, Bwana, kwa wale wanaowatunza wenye changamoto hii: wataalamu, wanafamilia, na wanaojitolea — wanaume kwa wanawake, ambao, kwa saburi na upendo, wanajenga madaraja ya uelewa na faraja.
Wakirimie nguvu na huruma waendelee kuhudumia wengine.
Tushushie Roho wako Mtakatifu, ili tujifunze kupokea na kujumuisha huduma ya afya ya akili katika maisha na utume wa jumuiya zetu na Kanisa lote, na hivyo kuwa ishara hai ya huruma yako, huruma isiyokoma kamwe, bali daima inaendelea kurejesha hali njema. Amina.