Sali na Papa

Historia Yetu

MAANA YA MTANDAO WA SALA WA BABA MTAKATIFU ULIMWENGUNI.

Mtandao wa Sala wa Baba Mtakatifu Ulimwenguni ni Ushirika wa Kipapa, wenye dhamira ya kuhamasisha Wakatoliki kupitia sala na matendo mema kukabili changamoto zinazoukabili Ulimwengu na Utume wa Kanisa. Changamoto hizi zinawasilishwa kwa njia ya Nia za Sala za kila mwezi anazokabidhi Baba Mtakatifu kwa Kanisa zima. Kwa kuzipokea nia hizi kwa sala, mawazo na matendo, wanachama wanaingiwa na huruma kwa ulimwengu wote, huruma yenye asili yake katika Moyo wa Yesu.

Lengo Letu

Mtandao wa Sala wa Baba Mtakatifu unakabili kwa sala na matendo changamoto za binadamu na za Utume wa Kanisa.

Nyenzo Zetu

Sala na matendo ya kukabiliana na changamoto zinazoukabili binadamu na Utume wa Kanisa kama inavyobainishwa na Baba Mtakatifu. Nia za sala za Baba Mtakatifu ni muhimu kwa sala na utume wetu.

Mbinu zetu

Kuwa mitume katika maisha ya kila siku, kupitia njia ya kiroho inayoitwa "Njia ya Moyo", ambayo hubadilisha maisha yetu kuwa kwa utumishi katika utume wa Kristo, utume wa huruma kwa ulimwengu.

HISTORIA YA UANZILISHI:

Mtandao wa Sala wa Baba Mtakatifu Ulimwenguni ulianza mwaka 1844 huko Vals, Ufaransa, wakati Padre Francis Xavier Gautrelet SJ alipowahimiza vijana Wajesuiti (Wajezuiti Walelewa) kuwa mitume na wamisionari hata wawapo masomoni. Vijana hawa walianza kuyafanya majukumu yao ya kawaida kuwa matoleo ya kiroho. Mazoezi haya hapo awali yalijulikana kama Utume wa Sala (Apostleship of Prayer), yakaonesha umuhimu wa kuishi maisha ya utayari wa kitume wa kudumu; na kuongeza thamani ya kiroho ya shughuli za kawaida kwa “kuziunganisha na Sadaka Takatifu ya Kristu” kupitia Ibada Takatifu ya Misa. Kwa njia ya majitoleo binafsi ya kila siku, kila siku utayari huu wa kitume ulipyaishwa Utume huu ulienea haraka hata nje ya nyumba za Wajesuiti. Kwa sasa unajumuisha zaidi ya Wakatoliki milioni 22 katika nchi 92, likiwemo tawi la vijana tunaloliita Vijana Wana Ekaristia (Eucharistic Youth Movement, EYM). Mwaka 2020, Mtandao wa Sala wa Baba Mtakatifu Ulimwenguni ulifanywa rasmi Shirika la Kipapa.

NAMNA ZA USHIRIKI:

Mtandao huu unatoa namna kuu tatu za kushiriki:.

01

Njia ya Wazi:

Mshiriki hawi mwanachama wa kikundi chochote, bali yeye mwenyewe hutafuta njia ya kusali kwa Nia ya Baba Mtakatifu na kufanya mazoezi mengine ya mtume wa sala.

02

Uanachama wa Kikundi cha Mitume wa Sala:

Mtu huwa mwanachama wa kikundi cha utume wa sala, kinachofuata taratibu, uongozi na kanuni za sehemu mahalia: utaratibu ya kiparokia, kijimbo, shule, chuo nk.

03

Kuwa katika Kikundi Wapenzi wa Utume wa Sala:

Hapa huwa kikundi kama Jumuiya Ndogo, Kwaya, shule nk. Ambacho hutumia sala za utume huu, japokuwa wao si kimundi maalum kwa utume huu.

MAZOEZI MUHIMU YA MTUME WA SALA

  • Kusali sala majitoleo ya kila siku: Utume huu una sala ya majitoleo ya Nafsi ya Kila siku. Ni vema majitoleo haya yakifanywa katika Ibada Takatifu ya Misa.
  • Kusali kwa nia ya sala ya Baba Mtakatifu: Baba Mtakatifu hutoa nia yake ya sala kila mwezi naye mwenyewe husali na Kanisa lote kwa nia hiyo kila Ijumaa ya Kwanza ya Mwezi.
  • Kuhudhuria Misa na Kupokea Ekaristi Takatifu: Msingi wa Utume huu ni upendo na huruma ya Kristo. Fumbo la Ekaristi Takatifu hubeba vema upendo huu wa kiungu na kuuleta katika maisha yetu ya kila siku ki-sakramenti.
  • Kufanya matendo ya upendo na huruma: Huku ni kujitahidi kufanya juhudi za makusudi za kuonesha huruma na mapendo kwa wahitaji.
  • Kujichunguza Rohoni: Katika vipindi vitatu vya siku: Asubuhi, Mchana na Jioni (au Usiku) Mtume wa Sala huchunguza nafsi yake, kujiweka katika utambuzi wa jinsi anavyotembea na Kristu na kushirikishwa utume wake.

Jiunge Nasi

kuwa sehemu ya Imani na Matumaini Ulimwenguni.